- NEWS & PUBLICATIONS

Back

Serikali Kuendelea Kuimarisha Ukusanyaji wa Mapato ya halmashauri

Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini zimetakiwa kuhakikisha kuwa fedha zote zinazokusanywa katika mapato zinawekwa benki kabla ya kupangiwa matumizi husika ili kuwa salama zaidi na kuhakikisha zinakwenda kutekeleza matumizi husika.

Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhandisi Joseph Nyamhanga katika hafla ya upokeaji wa mashine za kielektroniki (point of sales machines) kutoka Serikali ya Dernmark ofisini kwake Jijini Dodoma leo.

“Makatibu Tawala wa Mikoa kuweni makini katika ukusanyaji wa mapato ili kutimiza azma ya serikali ya kuongeza udhibiti na kuleta tija katika ukusanyaji wa mapato katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuhakikisha fedha ilokusanywa inahifadhiwa benki kabla ya matumizi yoyote”Amesema Mhandisi Nyamhanga.

Aidha, Mhandisi Nyamhanga ameongeza kuwa jitihada hizi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano zitasaidia kuongeza kipato katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, kupunguza mianya ya izi wa fedha, kupunguza utegemezi na kuboresha utoaji wa huduma za kijamii kwa wananchi.

Naye Mkurugenzi wa Serikali za Mitaa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt.Charles Muhina amesema kuwa hafla hiyo ya kukabidhi mashine hizo kwa mikoa hiyo ni mwendelezo wa kuziwezesha Halmashauri kuwafikia walipa kodi waliopo kwenye maeneo yao na kuongeza wigo katika ukusanyaji wa mapato katika maeneo yao.

“Sisi OR-TAMISEMI jukumu letu ni kufanya ufuatiliaji na tathimini ya utekelezaji wa mradi ili kuhakikisha kuwa mradi husika unatekelezwa kwa kuzingatia sheria, kanuni, na taratibu za nchi hii” Ameongezea Dkt. Muhina

Kwa upande wake Mkurugenzi wa TEHAMA Ofisi ya Rais TAMISEMI Erick Kitali ametoa wito kwa halmashauri kuwa na kifaa maalumu cha kuzuia radi ili kutatua changamoto ya mitandao ya mifumo ya mapato kaharibiwa radi kipindi cha mvua katika halmashauri hizo.

Awali Kiongozi wa Mradi Maboresho ya Mazingira ya Biashara Flemming Olsen ametoa wito kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano waTanzania kuhakikisha  mapato yanakusanywa kwa ufasaha kwani kuna wafanya biashara wanabidhaa ya thamani kubwa  lakini wanalipa ushuru mdogo.

Wakati huo huo Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma Rashid Mchatta amesema kuwa atakwenda kusimamia vyema mashine hizo ili zifanye kazi ipasavyo na itasaidia kuongeza mapato katika maeneo yao ya kazi.

Katika hafla hiyo Mhandisi Nyamhanga amehitimisha kwa kutoa shukurni za dhati  kwa niaba ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa wananchi wa Serikali ya Denmark kupitia Ubalozi wa Denmark nchini Tanzania na kusema kuwa ushirikiano wa nchi hizi mbili utaleta maendeleo kwa wananchi wa Tanzania kwa ujumla.

Makala nyingine zinaweza kupatikana kupitia : Ofisi ya Rais - Tamisemi iko kwenye Facebook  na Mwanahalisi